Jukwaa la Nasser la Kimataifa Lajadili Bandung, mabadiliko ya tabianchi na utawala bora

Jukwaa la Kimataifa la Nasser limetangaza, kupitia taarifa rasmi, kuandaa kikao cha majadiliano chenye kichwa: "Miaka 70 tangu Mkutano wa Bandung na Uundwaji wa Nchi za Ulimwenguni Kusini", kuadhimisha miaka 70 tangu kufanyika kwa mkutano huo, katika ufunguzi wa siku ya kumi na moja ya Toleo la Tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, unaofanyika chini ya Ufadhili wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa, chini ya kaulimbiu “Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi Masuala ya Ulimwenguni Kusini”, kwa ushiriki wa vijana viongozi 150 kutoka mataifa 80 duniani kote.
Dkt. Noha Bakr alisisitiza mchango wa vijana katika kuelimisha jamii zao hasa kuhusu magonjwa ya mlipuko, na kusema kuwa watu wetu wanastahili demokrasia na haki. Aliongeza kuwa janga la COVID-19 lilikuwa funzo muhimu, kama ilivyo kwa mabadiliko ya tabianchi, ambayo hayakusababishwa na mataifa yanayoendelea. Hivyo, alisisitiza kuwa mataifa makubwa lazima yachukue jukumu lao. Alielezea pia umuhimu wa vijana kushirikiana na mashirika ya kiraia, hasa wakati ambapo baadhi ya nchi kubwa zinapunguza ahadi zao, mfano uondoaji wa Marekani kutoka Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Katika hotuba yake wakati wa kikao cha majadiliano cha ufunguzi wa siku ya kumi na moja ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, Kundi la tano, Dkt. Noha El-Mekkawy alieleza kuwa Mkutano wa "Bandung" uligeuka kuwa misingi iliyoanza kutekelezwa katika miaka ya sitini. Akisisitiza umuhimu wa kupitia kumbukumbu za Umoja wa Mataifa ili kuelewa misingi ya haki ya kweli. Alitilia mkazo umuhimu wa mfumo wa uwingi wa kimawazo na imani katika dhana hiyo, pamoja na kuchunguza njia za kutekeleza demokrasia na kuimarisha misingi yake, huku akihimiza kubadili kanuni za zamani ili ziendane na hali halisi za kisasa na mabadiliko yanayoendelea. Alitoa wito wa kulinda taasisi za kidemokrasia na haki, na kuunga mkono mfumo wa mahakama na kuuhifadhi, badala ya kutegemea tu majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa kutoa maoni, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari na mabunge vimeshindwa kutekeleza majukumu yao ya msingi. Dkt. El-Mikawy alisisitiza pia juu ya haja ya kujenga jamii ya kiraia iliyo thabiti na endelevu, akieleza kuwa taasisi hizi ndizo zinazoakisi mawazo na ndoto ambazo vijana wanatamani kuzitimiza. Aidha, alibainisha kuwa Afrika ni bara lenye ukarimu na uwezo mkubwa, na hivyo ni wajibu wa nchi za bara hili kushikamana kwa pamoja ili kuubadilisha ulimwengu na kuunga mkono vyombo vya habari vinavyotafuta ukweli. Alisisitiza kuwa demokrasia inahitaji watetezi wa kweli, na kwamba kuimarisha mazungumzo kati ya vizazi ni jambo la lazima ili kuunganisha wadau wote na kufanikisha mabadiliko yanayotarajiwa.
Kwa upande wake, Hassan Ghazaly, mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa, alisema kuwa kikao hiki ni sehemu ya kuadhimisha miaka 70 ya Mkutano wa kihistoria wa Bandung, ulioweka msingi wa mshikamano waNchi za Ulimwenguni Kusini . Aliongeza kuwa kikao hicho kilichofanyika katika siku ya kumi na moja ya toleo la tano la Udhamini huu kililenga kutathmini tena misingi ya mkutano wa Bandung katika muktadha wa changamoto za kisasa. Alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa Kusini na mchango wa vijana katika kuunda mustakabali wa haki, ushirikiano na mfumo wa kimataifa ulio sawa na jumuishi.
"Jukwaa la Nasser la Kimataifa ": Kikao cha Majadiliano kuhusu "Tabianchi" katika Siku ya Kumi na Toleo la Tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimatifa
Jukwaa la Nasser la Kimataifa liliongeza katika taarifa yake kwamba kikao kingine cha majadiliano kilifanyika kwa kichwa: "Tabianchi Yetu", kama sehemu ya shughuli za siku ya kumi na moja ya Toleo la Tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimatifa, unaofanyika chini ya Ufadhili wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi na kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa, chini ya kaulimbiu “Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi Masuala ya Ulimwenguni Kusini ”, kikihudhuriwa na vijana viongozi 150 kutoka mataifa 80 duniani. Kikao hicho kiliendeshwa na Dkt. Mustafa Abbas, mjasiriamali wa kijamii na kiutamaduni, na Mkurugenzi wa Kituo cha "Wasla" mjini Berlin. Walihudhuria pia Mhandisi Walid Haqiqi, Mkuu wa Idara ya Mipango katika Wizara ya Rasilimali za Maji ya Misri na Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretarieti ya Kudumu ya Wiki ya Maji ya Kairo, pamoja na Dkt. Mariam Allam, mtaalamu wa athari za mabadiliko ya tabianchi na mshiriki katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
Majadiliano haya ya shughuli za siku ya kumi ya moja ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimatifa yalilenga changamoto zinazoikumba sekta ya maji nchini Misri kutokana na mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa rasilimali za maji. Washiriki walizungumzia juhudi za kitaifa za kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, usimamizi endelevu wa maji, na kuanzisha vituo vya kuchakata maji ya chumvi. Pia, walijadili matumizi ya mbinu za kisasa za umwagiliaji, kupunguza uchafuzi wa maji, na uwekezaji katika teknolojia za kuchakata maji, sambamba na Dira ya Misri ya Maji 2050 iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Rasilimali za Maji na Wizara ya Makaazi. Kikao pia kilisisitiza mchango wa Wiki ya Maji ya Kairo kama jukwaa la kimataifa la uhamasishaji na ushiriki wa mashirika ya kimataifa katika kuhifadhi rasilimali za maji. Washiriki walielezea mbinu za kitaifa na kimataifa, umuhimu wa kuhusisha vijana na mashirika ya kiraia katika kukabiliana na changamoto za tabianchi, na kujenga uwezo wa vijana kuelewa mchakato wa mazungumzo ya kimataifa hadi utekelezaji, pamoja na mbinu za kupata fedha za kufanikisha suluhisho endelevu.
Katika kikao cha majadiliano kwa anwani "Hali ya Hewa Yetu", Mhandisi Walid Hakiki, Mkuu wa Sekta ya Mipango katika Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji ya Misri, alieleza kuwa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ni mojawapo ya maeneo yanayokumbwa na uhaba mkubwa wa maji, jambo linalozilazimu nchi —ikiwemo Misri— kutafuta vyanzo vya fedha kukabiliana na changamoto hii. Alifafanua kuwa sekta ya kilimo nchini Misri ni mojawapo ya sekta muhimu inayotegemewa na idadi kubwa ya wafanyakazi, lakini kiwango cha mvua kinachoonesha nchini ni kidogo sana, na hakizidi asilimia 2 kwa mwaka—hii ni asilimia ya chini sana. Aidha, alieleza kuwa Misri, ikiwa ni nchi ya mwisho katika mtiririko wa Mto Nile, inaathirika sana na uhaba wa maji na tayari iko chini ya mstari wa umasikini wa maji. Hali hii inalazimu kuwepo kwa juhudi za kuziba pengo la maji ambalo limefikia takriban bilioni 2 za mita za ujazo kila mwaka. Akaongeza kuwa kuna mpango wa kitaifa wa usimamizi wa rasilimali za maji unaotegemea mkakati wa ushirikiano kati ya wizara mbalimbali ili kufanya kazi kwa pamoja kuhifadhi maji na kuendeleza vyanzo vyake. Akionesha kuwa kutegemea mitambo ya kusafisha maji ya chumvi na visima vya chini ya ardhi ni jambo lenye gharama kubwa sana.
Vilevile, Katika hotuba yake, alieleza kuwa serikali ya Misri inatekeleza mpango wa kitaifa wa kukuza uwezo wa kuhifadhi maji, pamoja na miradi ya kutibu maji taka, ambapo takriban bilioni moja ya mita za ujazo ya maji hutumika tena kila mwaka. Hata hivyo, bado kuna haja ya uwekezaji mkubwa kufanikisha miradi hii muhimu.
Alieleza pia kuwa serikali imeanzisha programu za kidijitali kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima na kuwapa taarifa muhimu kuhusu muda na kiasi cha maji kinachohitajika, pamoja na ufuatiliaji wa viashiria vya utendaji na kutoa majibu ya maswali yao kuhusu aina za mazao na nyakati mwafaka za kupanda. Aliangazia pia juhudi za serikali kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko, kufuatilia upungufu wa fukwe, na ukarabati wa mifereji kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira. Alibainisha kuwa "Wiki ya Maji ya Kairo" ambayo huandaliwa kila mwaka nchini Misri, sasa ni sehemu ya ratiba ya Wiki ya Maji Duniani kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kufikisha sauti ya Misri na nchi zinazoendelea kuhusu tatizo la uhaba wa maji kwenye jukwaa la kimataifa. Aliongeza kuwa Misri pia huandaa mafunzo kwa vijana wa Kiafrika ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa maji ya Mto Nile na haki za nchi zinazoshiriki katika Bonde lake.
Dkt. Mariam Allam, mtaalamu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, aliwaeleza washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimatifa kuwa Afrika haijachangia kwa kiwango kikubwa katika kusababisha tatizo la mabadiliko ya tabianchi, lakini ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi kutokana na shughuli za nchi kubwa zilizoendelea, ambapo mchango wa Afrika hauzidi asilimia 4 ya vyanzo vinavyosababisha mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa bara la Afrika lilikuwa mshiriki muhimu katika majadiliano ya kimataifa kuhusu tabianchi, lakini bado kuna hitaji la dharura kwa viongozi wa Afrika kuwajibika zaidi na kupeleka mbele hatua za kupata vyanzo vipya vya fedha. Alionya kuhusu uhaba wa wataalamu wa Kiafrika wenye uwezo wa kubuni miradi itakayovutia ufadhili kutoka taasisi za kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kutumia akili bandia na teknolojia ya kisasa kuboresha matokeo katika sekta za uhandisi wa fedha na kupunguza mzigo wa madeni unaolipambana bara la Afrika kutokana na changamoto za kijiografia na ukosefu wa fedha za umma.
Alisisitiza pia haja ya kuwepo kwa mipango ya kifedha ya kweli na inayotekelezeka, na kuimarisha mchango wa sekta binafsi ambayo inakumbwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pia, alielezea kwamba Wizara ya Vijana na Michezo ya Misri inawaunga mkono vijana wanaoshiriki katika Mkutano wa Vijana kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, lakini bado kuna haja ya msaada zaidi ili kuonesha juhudi na mawazo ya vijana pamoja na suluhisho endelevu wanazopendekeza. Akieleza kuwa Misri imeanzisha mpango wa “Maisha Bora (Haya Karima)” kwa lengo la kuongeza uwezo wa wakazi wa vijijini, kuboresha miundombinu, kuhifadhi maji na kuboresha matumizi ya nishati. Alihimiza washiriki kuunga mkono viwanda vinavyozingatia kanuni za maendeleo endelevu, kutumia bidhaa zinazoweza kutumika tena, na kuepuka bidhaa zinazoharibu mazingira, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kweli huanza na mtu binafsi.
Kwa upande wake, Hassan Ghazaly, Mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa, alisema kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi haipaswi kuchukuliwa kama suala la mazingira tu, bali ni suala la maendeleo na haki za kibinadamu, linaloathiri moja kwa moja mustakabali wa watu, hasa katika nchi zinazoendelea na barani Afrika —ambayo haikuchangia sana katika kuileta hali hii lakini inabeba sehemu kubwa ya athari zake. Vilevile, alisisitiza kuwa maudhui ya kikao hicho yanaonesha umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja, na haja ya kuunda mbinu mpya za kifedha zitakazowezesha nchi za Kusini kutekeleza suluhisho halisi na endelevu. Alisema kuwa vijana ndio kiini cha mabadiliko haya, kupitia matumizi ya teknolojia na kutoa mawazo mapya yanayoweza kuongeza uimara wa jamii katika kukabiliana na majanga ya kimazingira. Aidha, aliongeza kuwa udhamini wa Nasser unafungua milango kwa ajili ya majadiliano, kujifunza, na kazi ya pamoja, na hivyo kuchangia katika kuwajengea uwezo kizazi kipya cha viongozi wanaoweza kutetea masuala ya Kusini Globali, kudai haki ya tabianchi, na kujenga mustakabali wenye usawa na maendeleo endelevu.
"Jukwaa la Nasser": Haki, Utawala na kupambana Ufisadi – Mjadala wa Mwisho wa Siku ya Kumi na Moja
Pia, Jukwaa la Nasser la Kimataifa lilitangaza kupitia taarifa yake kwamba limeandaa kikao cha majadiliano kilichobeba kichwa: "Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Ufisadi", katika kuhitimisha shughuli za siku ya kumi na moja ya toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, unaofanyika mwezi Mei huu chini ya kauli mbiu “Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi Masuala ya Ulimwenguni Kusini ”, kwa Ufadhili wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Kikao hicho kilihudhuriwa na zaidi ya vijana 150 wa kike na wa kiume kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwa ni viongozi vijana kutoka sekta na taaluma mbalimbali, pamoja na vijana mashuhuri wenye ushawishi katika jamii zao.
Kikao cha majadiliano kiliongozwa na Dkt. Ashraf Sobhy, Waziri wa Vijana na Michezo, kwa kushirikiana na Alaa El-Din El-Desouky, Naibu Waziri na Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Vijana, na Hassan Ghazaly, Mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa, pamoja na viongozi wengine wa Wizara ya Vijana na Michezo. Kikao hiki kilihudhuriwa na kundi la wataalamu mashuhuri kutoka Mamlaka ya Ukaguzi wa Utawala na Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi: Luteni Jenerali Dkt. Mohamed Salama, Naibu wa Kwanza wa Mamlaka ya Ukaguzi wa Utawala na Mshauri wa Rais wa Mamlaka hiyo kuhusu masuala ya Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi; Bwana Ayman Abou El-Ala, mjumbe wa Mamlaka ya Ukaguzi wa Utawala na Msaidizi wa Rais wa Muungano wa Taasisi za Afrika za Kupambana na Ufisadi; na Bwana Emad Zaghloul, mjumbe wa Mamlaka hiyo na mhadhiri katika Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi. Wataalamu hao walijadili juhudi za Misri katika kupambana na ufisadi, mkakati wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ufisadi, changamoto kuu, mifano ya mafanikio, pamoja na mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusiana na mapambano haya.
Kikao cha majadiliano kilichoandaliwa kufunga shughuli za siku ya kumi na moja ya Toleo la tano la udhamini wa Naseer kwa Uongozi wa Kimataifa, chini ya kichwa “Utawala na Mapambano Dhidi ya Ufisadi,” kiliendeshwa na Dkt. Hussein Bassiouny. Katika mwanzo wa hotuba yake, alieleza kuwa suala la kupambana na ufisadi na kuimarisha utawala bora ni jambo msingi linaloathiri moja kwa moja mustakabali wa maendeleo na utulivu. Alibainisha kuwa Misri ilitambua mapema umuhimu wa mada hii, na hivyo kuanza kutekeleza mikakati madhubuti na mipango ya kukabiliana na changamoto hiyo. Pia, alieleza kuwa serikali ya Misri imezindua Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi, unaolenga kukuza uwazi, kuboresha sheria, na kuwezesha taasisi za udhibiti. Licha ya maendeleo yaliyopatikana, changamoto bado zipo – zikiwemo kukuza utamaduni wa uwajibikaji wa kijamii, kupambana na urasimu wa kiutawala, na kusasisha mifumo ya usimamizi wa serikali. Alisisitiza kuwa mafanikio ya Misri katika baadhi ya sekta yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa, na akasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kupitia kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya msaada wa kisheria, ili kujenga mfumo jumuishi wa utawala bora unaosaidia kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Kwa upande wake, Waziri wa Vijana na Michezo, Dkt. Ashraf Sobhy, aliwakaribisha wataalamu kutoka Mamlaka ya ufuatiliaji wa ufisadi, na kueleza kuwa mhadhara huu ni kati ya mihadhara ya muhimu sana; kwani unazungumzia dhima kuu ya serikali na ushirikiano kati ya sekta za serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi. Alieleza kuwa dhana ya utawala bora inajumuisha maadili kama vile uadilifu, uwazi, na uwajibikaji, pamoja na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha usimamizi thabiti. Vilevile, alieleza kuwa wizara yake inashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi, ambayo ni mshirika hai katika kukuza dhana ya utawala bora katika jamii ya Misri. Alipongeza juhudi za Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi ambacho huandaa kozi za mafunzo na mazoezi kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine, kwa lengo la kukuza uelewa na kujenga uwezo. Alihitimisha kwa kusema kuwa mkutano huu ni fursa muhimu ya kuonesha juhudi za kitaifa za kupambana na ufisadi, na kuhimiza ushirikiano kati ya pande zote ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Kwa upande mwingine, Meja Jenerali Daktari Mohamed Salama, Naibu Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi, alieleza furaha yake kushiriki kwenye kikao hiki muhimu. Aliwasilisha salamu kutoka kwa Meja Jenerali Amr Adel – Mkuu wa Mamlaka – pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi. Katika mada yake iliyopewa jina “Nafasi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi katika Kuzuia na Kupambana na Ufisadi”, alieleza kuwa dhana ya ufisadi si mpya, bali imekuwepo tangu mwanzo wa historia ya binadamu, na ilijitokeza hata kwenye ustaarabu wa kale. Akiweka wazi kuwa ustaarabu wa Kigiriki uliiga baadhi ya dhana kutoka kwa ustaarabu wa Misri ya Kale, ambapo mwanafalsafa Plato alizungumzia uadilifu kama sifa muhimu kwa watumishi wa umma. Pia, aliongeza kuwa dini za mbinguni – hasa Qur’ani Tukufu – zimeelezea mara nyingi madhara ya ufisadi. Pia alimtaja Ibn Khaldun, mwasisi wa sayansi ya jamii, aliyetoa mtazamo wa kijamii kuhusu ufisadi, akieleza kuwa ufisadi huathiri sio tu taasisi za serikali, bali hata watu binafsi na jamii kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Meja Jenerali Daktari Salama alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi na Chuo cha Kitaifa, ufisadi unafafanuliwa kama “matumizi mabaya ya mamlaka kwa ajili ya kupata manufaa binafsi”. Alichambua aina mbalimbali za ufisadi: wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutawala; pamoja na viwango vyake, kuanzia wa ndani hadi wa kimataifa, na ukubwa wake kuwa mdogo au mkubwa. Alielezea pia athari mbaya za ufisadi katika ngazi ya sheria, jamii, uchumi na siasa. Zaidi ya hayo, alielezea Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi, muundo wake wa kitaasisi, na makosa ya jinai ambayo mamlaka hiyo inashughulikia. Akitoa muhtasari wa kampeni mbalimbali za elimu na uhamasishaji zilizoanzishwa na mamlaka hiyo ili kueneza utamaduni wa uwazi na uadilifu. Kikao kilihitimishwa kwa kuoneshwa kwa filamu ya maandishi (documentary) kuhusu kazi ya mamlaka hiyo na mchakato wa kupokea wanachama wapya.
Katika hotuba yake, Meja Jenerali Daktari Mohamed Salama, Mshauri wa Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi kuhusu masuala ya Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi, alielezea juhudi za chuo hicho katika nyanja za mafunzo, uandaaji na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu wa kitaifa wenye uwezo wa kukabiliana na aina zote za ufisadi. Alibainisha kuwa chuo hicho kilianzishwa kwa udhamini wa urais kama mkono wa mafunzo wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi, kikilenga kuwa rejea kuu ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika elimu na mafunzo ya kuzuia na kupambana na ufisadi, kwa kutumia mifumo ya kisasa ya mafunzo. Akieleza kuwa chuo hicho kinatoa huduma mbalimbali za kielimu na mafunzo, ikiwa ni pamoja na masomo ya juu, utafiti, programu za mafunzo, warsha, mifano ya majaribio, na programu za kitamaduni, pamoja na shughuli za nje na kozi maalumu. Pia alitaja ushirikiano wa kweli uliopo kati ya chuo na taasisi za ndani, kikanda na kimataifa, katika muktadha wa kupanua wigo wa chuo hicho na kutimiza malengo yake ya baadaye ya kujenga jamii yenye uwazi na uadilifu.
Meja Jenerali Daktari Salama aliongeza kuwa taasisi hiyo huwalenga makundi mbalimbali ya jamii kama sehemu ya maono yake ya kusambaza utamaduni wa uadilifu na uwazi. Alifafanua kuwa programu za chuo zinajumuisha watumishi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi na maafisa wa utekelezaji wa sheria, pamoja na kozi fupi na za muda wa kati kwa maafisa wa serikali kutoka taasisi mbalimbali. Pia, alieleza kuwa chuo kinatoa kipaumbele kwa vijana, wanafunzi, watu wenye ulemavu na wanawake, kupitia ushirikiano na Baraza la Kitaifa la Wanawake na mashirika ya kiraia, na hutoa mafunzo ya jioni baada ya saa za kazi rasmi. Alibainisha kuwa chuo kinaandaa shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo ushiriki wa kila mwaka kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Kairo, pamoja na kutoa mafunzo katika mikoa ya Kusini na Kaskazini mwa Misri na vyuo vikuu, sambamba na kupokea wajumbe kutoka nchi za Kiarabu na Afrika katika programu za mafunzo ya hali ya juu, Jambo linalokifanya chuo kuwa jukwaa la kitaifa, kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya ufisadi na ujenzi wa uwezo.
Kupitia shughuli za siku 11 ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa kiamatifa, Katika hitimisho la hotuba yake, Naibu Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi alizungumzia nafasi ya vyombo vya habari na mashirika ya kiraia katika mapambano dhidi ya ufisadi, jambo linaloonekana wazi katika lengo la nne la kundi la tatu ya Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi, linalohimiza usambazaji wa maadili na kukuza uelewa wa kijamii kuhusu umuhimu wa kupambana na ufisadi. Alieleza kuwa kuwezesha taasisi za udhibiti kutekeleza majukumu yao kunategemea mambo mawili muhimu: kuwepo kwa nia ya kweli ya kisiasa, na uhuru wa kifedha, kiutawala na kitaalamu kwa taasisi hizo. Kwa kuzingatia kuwa ufisadi ni uhalifu wa mipaka unaoathiri jamii zote, alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni jambo la lazima, ambapo nchi hushirikiana kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya pamoja ya kupambana na ufisadi kwa ufanisi.
Pia katika hoyuba yake wakti wa shughuli hizo, Bwana Ayman Abou El-Ela, Mjumbe wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi na Msaidizi wa Rais wa Muungano wa Mamlaka za Kupambana na Ufisadi Afrika, alieleza kuwa Sekretarieti ya Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Kuzuia na Kupambana na Ufisadi, chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu, ndiyo yenye jukumu la kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kitaifa na kuratibu kazi kati ya taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya ufisadi nchini. Kamati hiyo ilianzishwa mwaka 2014 sambamba na uzinduzi wa awamu ya kwanza ya Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi. Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi si jukumu la taasisi au wizara moja pekee, bali ni wajibu wa pamoja wa jamii nzima – kwa taasisi zake na watu binafsi. Alifafanua kuwa mwaka 2014, Misri iliweza kuweka dira yake ya kwanza ya kitaifa ya kukabiliana na ufisadi, ambayo imeendelea kuimarika kupitia ushirikiano wa kimataifa na uanachama wake kwenye mikataba ya kikanda na kimataifa inayohusiana na mapambano hayo, jambo ambalo limeimarisha mipango ya kimkakati ya kitaifa ya kupambana na ufisadi.
Vilevile, aliongeza kuwa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi imefuata mbinu shirikishi katika kutengeneza na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Ufisadi, kwa kushirikiana na jamii ya kiraia, sekta binafsi, wizara, vyuo vikuu, wasomi na wafanyabiashara. Ushirikiano huu umeongeza ufanisi wa juhudi za kitaifa. Takriban 86% ya malengo ya awamu ya pili ya mkakati huo, ambayo ilitekelezwa kati ya 2019 hadi 2023, yamekamilika, na kipindi hicho kilishuhudia maendeleo makubwa katika utendaji wa taasisi na uratibu wa pamoja. Awamu ya tatu ya mkakati, iliyoanza 2024 na itaendelea hadi 2030, inakwenda sambamba na Dira ya Misri 2030, ikilenga kutoa dira mpya iliyoendelezwa ya jamii isiyo na ufisadi na yenye maadili ya uadilifu. Idadi ya malengo ya kimkakati imepunguzwa hadi malengo matano makuu yenye mwelekeo mahsusi, ili kuongeza ufanisi na kufanikisha matokeo ya kweli katika mazingira ya kitaifa safi na yenye uwezo wa kupambana na ufisadi kwa njia pana na madhubuti.
Kwa upande wake, Bwana Emad Zaghlef, Mjumbe wa Mamlaka ya Kudhibiti Ufisadi na Mhadhiri katika Chuo cha Kitaifa cha Kupambana na Ufisadi, alieleza wakati wa shughuli za udhamini huo pia kuwa Misri inatekeleza mbinu mahsusi na ya kina katika mapambano dhidi ya ufisadi, inayojikita katika utendaji wa taasisi na uratibu wa kimfumo kati ya taasisi husika. Alibainisha kuwa Misri ilikuwa kati ya nchi za mwanzo kujiunga na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ufisadi, pamoja na mkataba wa Afrika, mkataba wa Kiarabu, na Mkataba wa Makka wa Nchi za Ushirikiano wa Kiislamu, jambo linaloonesha dhamira ya kweli ya serikali ya kushirikiana kimataifa katika uwanja huu muhimu. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni wa lazima katika kupambana na ufisadi, kwa kuwa ni uhalifu wa kimataifa unaoathiri jamii zote bila ubaguzi.
Zoghlf, katika hotuba yake, alieleza kuwa ushiriki wa Misri katika mikutano na makongamano ya kimataifa umeipa nafasi nyingi za kuanzisha mbinu mpya za kupambana na ufisadi. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuanzishwa kwa vikundi vya majadiliano vinavyosaidia kubadilishana maarifa na uzoefu na nchi nyingine duniani, jambo limeloongeza hadhi ya Misri kama mshirika anayeaminika. Alibainisha kuwa baadhi ya nchi zimeanza kuomba rasmi msaada wa Misri katika kuandaa mikakati yao ya kitaifa, kuratibu mikutano, na kutekeleza vipengele maalumu vya mipango yao ya kupambana na ufisadi, pamoja na kutoa msaada wa kiufundi na kiteknolojia. Aidha, aliongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni matokeo ya juhudi za pamoja za kitaasisi zinazoakisi dhamira ya kisiasa ya wazi. Alisisitiza kwamba kupambana na ufisadi ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano endelevu wa kimataifa ili kufanikisha mazingira salama na yenye haki ya maendeleo.
Mjadala huo wa kisera ulihitimisha shughuli za siku ya kumi na moja ya toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, ambapo washiriki walitoa maswali na michango muhimu. Mshiriki mmoja kutoka Algeria alieleza kuwa utamaduni wa kuripoti vitendo vya ufisadi ni alama ya raia mwenye uelewa, lakini changamoto kubwa ni uwepo wa sheria madhubuti za kuwalinda watoa taarifa wa ufisadi. Kwa upande mwingine, mshiriki kutoka Ghana alisisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati madhubuti ya kupambana na ufisadi, ikianzia na ufafanuzi sahihi na wa wazi wa dhana ya ufisadi yenyewe, kwa kuwa ndiyo msingi wa ufanisi wa mkakati wowote wa kitaifa.
Katika hitimisho la kikao hicho, Waziri wa Vijana na Michezo, Dkt. Ashraf Sobhy, aliwashukuru na kuwapongeza wazungumzaji kwa ushiriki wao wenye thamani na kwa kuangazia mojawapo ya nguzo kuu za ujenzi wa taifa la kisasa ambayo ni kuimarisha misingi ya uwazi na utawala bora. Alisisitiza kuwa kikao hicho kiliwasilisha mtazamo jumuishi kuhusu juhudi za Misri katika uwanja huu, kwa kuonesha mfano wa kipekee wa Misri ndani ya muktadha wa Jamhuri Mpya inayolenga kuleta mageuzi ya kina katika sekta mbalimbali. Aidha, alieleza kuwa anathamini maarifa, uzoefu na mafunzo yaliyowasilishwa katika muhadhara huu muhimu, umeoonesha kwa dhahiri umuhimu wa kushirikiana kati ya taasisi za kitaifa na kimataifa katika kupambana na ufisadi na kujenga mfumo madhubuti wa kiutawala. Alithibitisha kuwa wizara itaendelea kuunga mkono matukio kama haya yenye lengo la kuongeza uelewa, kuwawezesha watendaji wa kitaifa, na kukuza utamaduni wa uadilifu na uwajibikaji katika jamii.