"Waziri Mkuu" apokea vijana 150 kutoka nchi 80 katika siku ya tatu ya toleo la tano la "Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa"

"Waziri wa Mambo ya Nje na Uhamiaji" ahudhuria mdahalo wa kisiasa kwa mada ya "Misingi ya Sera za Kigeni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa" mwishoni mwa shughuli za siku ya 3 za udhamini huo, akiambatana na Waziri wa Vijana na Michezo
Mdahalo wa wazi kwa mada ya "Azimio la Mustakabali: Matumaini na Malengo" kwa ushiriki wa Balozi Amr Aljoweily
Shughuli za siku ya tatu ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa(toleo la tano), zilianza kwa mdahalo wenye kichwa cha habari: "Azimio la Mustakabali: Matumaini na Malengo". Hafla hii, iliyo chini ya ufadhili wa Rais Abdel Fattah El-Sisi, ilifanyika kwa kauli mbiu: "Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilisha masuala ya Ulimwenguni Kusuni." Wakihudhuria vijana takriban 150 kutoka nchi mbalimbali duniani, mdahalo huo uliwashirikisha viongozi vijana kutoka sekta mbalimbali, pamoja na baadhi ya vijana waliothibitisha ushawishi mkubwa katika jamii zao.
Balozi Amr El-Goweily, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa ya Pande Nyingi na Usalama wa Kimataifa, alitoa salamu za makaribisho kwa washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, wakati wa ufunguzi wa shughuli za siku ya tatu ya Udhamini huo, na kupongeza ushiriki wao katika Udhamini huu muhimu. Akisisitiza haja ya kufanya mageuzi ya kimuundo na kitaasisi katika Umoja wa Mataifa, ili kuimarisha ufanisi na tija ya taasisi hiyo na kuhakikisha uwezo wake wa kushughulikia changamoto za dunia za sasa.
Pia alieleza kuwa Umoja wa Mataifa hauhusiani tu na vyombo vyake vikuu kama Baraza Kuu, Baraza la Usalama, na Mahakama ya Haki ya Kimataifa, bali unaenea zaidi kupitia mfumo mpana wa mashirika maalum kama Umoja wa Mawasiliano wa Kimataifa (ITU) na Shirika la Nishati ya Nyuklia la Kimataifa (IAEA), ambalo linaathiri maisha ya kila siku ya watu. Akibainisha kuwa "Mkataba kwa Ajili ya Mustakabali" unajadili masuala muhimu kama maendeleo endelevu, ufadhili wa maendeleo, mabadiliko katika uongozi wa dunia, masuala ya vijana, kizazi kijacho, na maendeleo ya kidijitali. Aliongeza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizindua vikundi sita vya kazi vinavyoshughulikia maeneo haya pamoja na kipengele maalum cha mageuzi ya taasisi. Alihimiza washiriki wa Udhamini huo kushiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali, kwa kuwa wao ni kizazi kinachoelewa teknolojia hizi kwa undani zaidi.
Pia, El-Goweily alisisitiza umuhimu wa kutazama mageuzi kwa mitazamo miwili: ufanisi (matumizi bora ya rasilimali) na uwezo wa kupata matokeo. Akisisitiza umuhimu wa mpango wa “UN 80” wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuongeza ufanisi wa mfumo wa Umoja wa Mataifa. Alisisitiza pia haki ya bara la Afrika kuwa na uwakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, likiwa bara pekee lisilo na kiti cha kudumu licha ya dhuluma za kihistoria ilizopitia. Alisema kuwa madai ya Afrika sasa ni kipaumbele ndani ya Mkataba wa Mustakabali.
Kwa upande wake, Maria Ibolitova kutoka Kazakhstan alieleza uzoefu wake katika shughuli za misaada na maendeleo endelevu, hasa kwa watoto na vijana. Alieleza kuwa alianza mradi wake wakati wa mlipuko wa COVID-19, kipindi ambacho shughuli zote za elimu na burudani zilifungwa, lakini watoto wenye mahitaji maalum walionyesha uhitaji mkubwa. Aliongeza kuwa japo hali kwa sasa ni dhaifu, wao wanaendelea kusaidia watoto, vijana na kujitolea ili kuharakisha utekelezaji wa maendeleo endelevu kupitia misaada yenye mchango halisi.
Norullah Turambetov, mhadhiri katika Mpango wa UNESCO wa Masomo ya Kulinganisha ya Dini za Dunia katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Kimataifa nchini Uzbekistan, alieleza shukrani zake kwa waandaaji wa Udhamini wa Nasser kwa kumpa nafasi ya kushiriki katika kikao hiki muhimu cha majadiliano, akieleza kuwa ni heshima kubwa kwake kutoa hotuba hii mbele ya vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Akieleza pia jukumu kuu la mazungumzo baina ya dini katika kuimarisha malengo ya "Mkataba kwa Ajili ya Mustakabali", ambao ni makubaliano ya kimataifa ya kina na yenye malengo makubwa, yanayolenga kushughulikia changamoto zinazohusiana ambazo dunia yetu inakabiliana nazo kwa sasa, na kuchangia katika kujenga dunia yenye haki zaidi, amani, na maendeleo endelevu. Mkataba huu unasisitiza tena kujitolea kwa haki za binadamu, haki ya kijamii, usawa wa kijinsia, elimu jumuishi, na mshikamano kati ya vizazi. Alikumbusha pia kwamba elimu na mazungumzo si tu nyenzo za maendeleo, bali ni msingi wa kuishi kwa amani na kusonga mbele kwa pamoja katika dunia iliyounganishwa. Aidha, alisisitiza katika hotuba yake kwamba Mpango wa UNESCO wa Masomo ya Kulinganisha ya Dini za Dunia katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Kimataifa nchini Uzbekistan una nafasi ya kipekee kuchangia katika vipaumbele hivi vya kimataifa kupitia utafiti wa kitaaluma, elimu ya tamaduni mbalimbali, na ushiriki wa vijana. Kwa kukuza uelewa na ushirikiano kati ya dini, tunachangia katika kujenga jamii zenye mshikamano na kukuza utamaduni wa amani.
Waziri Mkuu aliendelea kusema: “Mmetoka katika nchi mbalimbali ili kujiunga na toleo la tano la Udhamini wa Uongozi wa Nasser ambao ulianzishwa mnamo mwaka 2019 ukiwa ni Udhamini wa kwanza wa vijana wa Kiafrika, chini ya uenyekiti wa Misri katika Umoja wa Afrika. Baadaye ulipanuka kufikia mabara ya Asia, Australia, Amerika ya Kusini na Ulaya, pamoja na Afrika. Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa huu ni aina ya ushirikiano kati ya nchi za Kusini, si tu mpango wa Kiafrika.” Akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, idadi ya washiriki imefikia washiriki 600 kutoka nchi 90, na mpango huu umeshirikiana na taasisi 34 na mashirika ya kitaifa, bara na kimataifa. “Tunajivunia mafanikio haya, na tunafurahi kwa kushiriki kwa idadi kubwa ya viongozi vijana kutoka zaidi ya nchi 80 duniani kote, chini ya ufadhili wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri.”
Pia, Waziri Mkuu Dkt. Mostafa Madbouly, katika hotuba yake kwa washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, alisema kuwa Misri ilishiriki katika kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1945, na tangu wakati huo imekuwa na jukumu muhimu katika kuunga mkono masuala ya nchi zaUlimwenguni Kusini. Alisisitiza kuwa Misri imekuwa na mtazamo wa kuunganisha kati ya kujitolea kwake kwa misingi ya haki ya kimataifa na kutafuta maendeleo endelevu kwa ajili yake na kwa watu wa nchi zinazoendelea. Aliendelea kusema kuwa Misri imeelewa daima umuhimu wa Umoja wa Mataifa kama jukwaa la kimataifa la kutetea masuala ya nchi zinazoendelea. Hata hivyo, licha ya mafanikio yaliyopatikana, nchi hizi bado zinakumbwa na changamoto kubwa kama vile umaskini, mabadiliko ya tabianchi, na ukosefu wa usawa wa kiuchumi. Alisisitiza kuwa ni lazima kuimarisha nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na changamoto hizi kwa kuleta mageuzi katika taasisi za kimataifa ili kuhakikisha uwakilishi wa haki zaidi kwa nchi za Kusini katika kufanya maamuzi ya kimataifa, pamoja na kuimarisha mifumo ya ufadhili endelevu ili kusaidia miradi ya maendeleo, na kuwawezesha vijana kama viongozi wa baadaye wenye maono ya ukuaji na maendeleo. Dkt. Madbouly alisisitiza kuwa Misri inaamini katika ushirikiano wa pande nyingi, na inafanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa kutekeleza mikakati ya maendeleo endelevu. Serikali ya Misri inalenga kufanikisha maendeleo jumuishi na endelevu kupitia majukwaa madhubuti yanayochangia ukuaji, haki za binadamu, usalama, na amani ya dunia na kikanda.
Katika hotuba yake, Dkt. Mostafa Madbouly alieleza kuwa Misri inaendelea na juhudi zake za kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika nyanja za ulinzi wa amani na ujenzi wa amani, hasa kwa kuzingatia ushiriki mpana wa Misri katika operesheni za ulinzi wa amani, na pia kwa kuandaa Kituo cha Umoja wa Afrika cha Ukarabati na Maendeleo Baada ya Migogoro, pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Kairo cha Utatuzi wa Migogoro na Ulinzi wa Amani.
Waziri Mkuu aliangazia pia changamoto kubwa na za kipekee ambazo zinakabili eneo hilo, na athari zake kwa uchumi wa Misri, akisema: “Mnaweza kufuatilia yanayoendelea katika Bahari Nyekundu na jinsi hali hiyo ilivyoathiri vibaya mzunguko wa usafiri wa majini kupitia Mfereji wa Suez, hali iliyosababisha kupotea kwa zaidi ya 70% ya mapato ya mfereji huo. Bila shaka, hili limeathiri pia biashara ya kimataifa.”Akaongeza: “Mbali na hayo, mnafuatilia pia yanayotokea Gaza, Sudan, Libya na nchi nyingine zinazopitia hali ngumu ya kutafuta utulivu. Katika hali hii, Misri inacheza jukumu muhimu kupitia juhudi za upatanisho kwa ajili ya kusitisha mapigano katika nchi hizi, ambazo ni majirani wa moja kwa moja na zina athari ya moja kwa moja kwa usalama na uthabiti wa Misri.”
Katika hotuba yake, Dkt. Madbouly alieleza kuwa kutokana na changamoto hizi za kikanda, Misri inawakaribisha zaidi ya wahamiaji na wakimbizi milioni 10, idadi inayozidi hata idadi ya wakazi wa baadhi ya nchi. Alitoa wito kwa washiriki kufikiria jinsi Misri inavyojitahidi kuwahudumia watu hawa kwa kuwapa huduma za msingi na mahitaji ya kibinadamu. Hili ni sehemu ya utamaduni wa watu wa Misri, ambao hawasiti kamwe kuwasaidia wanaohitaji msaada. Alifafanua kuwa licha ya changamoto hizi zote, Misri inaendelea kufanya juhudi kubwa za kuboresha hali ya kiuchumi, ambapo serikali imechukua hatua jasiri za mageuzi ya kiuchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji, na kuchochea ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, iwe ni kwa uwekezaji wa kigeni au wa ndani. Aliongeza kuwa Misri imeweza kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa miaka ya hivi karibuni, na sasa inafanya juhudi kuvutia zaidi uwekezaji katika nyanja mbalimbali.
Katika muktadha huu, Waziri Mkuu aliwaalika wageni waliokuwepo kufikiria kuhusu nchi ambayo idadi ya watu huongezeka kwa watu milioni mbili kila mwaka, jambo ambalo linahitaji kuunda takriban nafasi milioni moja za ajira kila mwaka – changamoto kubwa kwa serikali yoyote inayojitahidi kutoa mahitaji hayo kwa wananchi wake. Aliongeza kuwa licha ya changamoto hizo, Misri imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupambana na ukosefu wa ajira, ambapo kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua hadi asilimia 6.5% kutoka 13.5% mnamo mwaka 2014, licha ya ongezeko la watu milioni 18 katika kipindi hicho. Serikali imeweza kushughulikia ongezeko hilo huku ikipunguza ukosefu wa ajira.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa mafanikio haya yametokana na uongozi wa Rais Abdel Fattah El-Sisi, ambapo ilianzishwa Dira ya Misri 2030, na mafanikio makubwa yalipatikana katika sekta za makazi, vituo vya vifaa (logistics), huduma za kiuchumi na kijamii. Aliongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado kuna kazi kubwa mbele yao kwa sababu changamoto ni kubwa na tata, hasa kutokana na hali katika nchi jirani na eneo kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alieleza kuwa hali sasa imekuwa bora kwa kiwango kikubwa, na kwamba wanafanya juhudi kubwa kufikia malengo yaliyowekwa kwa manufaa ya wananchi na uchumi wao. Aliongeza kwa kusema: "Tunaamini kuwa katika mazingira haya ya ukosefu wa utulivu katika eneo letu, mikusanyiko ya aina hii inayowaleta pamoja viongozi wa baadaye ni msingi mzuri kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano chanya baina yenu. Ninasimama mbele ya watu kutoka Asia, Amerika Kusini, na hata Ulaya. Uwepo wenu hapa leo utawasaidia kuelewa vyema hali halisi ya eneo hili na bara la Afrika. Na hivyo, mtakapokuwa viongozi wa baadaye wa nchi zenu, mtakuwa na mtazamo mpana na wa uelewa zaidi kuhusu eneo letu na dunia kwa ujumla."
Dkt. Mostafa Madbouly aliongeza: "Hili litasaidia katika kukuza mahusiano ya kibinadamu kati ya mabara na mataifa mbalimbali. Ninyi kama viongozi vijana mnaakisi matumaini ya binadamu. Kwa hiyo, mikusanyiko ya aina hii ni muhimu sana. Mimi binafsi nimeshiriki katika majukwaa kama haya na imenisaidia sana kubadilisha mtazamo wangu, fikra zangu, na kunifanya niwe mtu mwenye maono ya pamoja na wa kushirikiana zaidi. Imenisaidia kuelewa tabia na miitikio ya watu. Kwa hivyo, mikutano kama hii ni muhimu kwa kujenga mahusiano kati ya mataifa na kati ya viongozi wa mustakabali."
Waziri Mkuu alisema pia: "Ninayo furaha kuwakaribisha hapa nchini Misri. Na kwa kuwa mmepata nafasi ya kutembelea mji mkuu mpya wa utawala, naamini mmepata fursa ya kuona mji huu. Sehemu hii ilikuwa jangwa tupu miaka minane iliyopita, lakini leo hii mlichokiona ni ushahidi tosha kwamba Wamisri ni wajenzi wa kweli — tangu majengo ya piramidi hadi mji huu mpya wa kiutawala. Wamisri daima wamekuwa watu wa maendeleo na si wa uharibifu, vita au mapigano. Hii ni sehemu ya asili ya Mmisri: tunapenda amani, tunatafuta ujenzi, na tunachukia migogoro."
Dkt. Mostafa Madbouly alihitimisha hotuba yake kwa washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa kwa kusema: "Kwa mara nyingine, nawakaribisha kwa moyo mkunjufu na ninawatakia mkutano mwema hapa Misri. Ninamwomba Waziri wa Vijana na Michezo kuhakikisha mna makazi bora na huduma nzuri ili muweze kufahamu vyema maendeleo yanayoendelea hapa nchini."
Dkt. Badr Abdel Aaty, Waziri wa Mambo ya Nje na Uhamiaji, alishiriki katika mdahalo wenye kichwa: "Misingi ya Sera ya Mambo ya Nje kwa Mujibu wa Umoja wa Mataifa", akihitimisha shughuli za siku ya tatu za "Nasser Fellowship for International Leadership" chini ya udhamini wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi kwa kauli mbiu: "Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi Masuala ya Ulimwenguni Kusini."
Katika hotuba yake, Waziri huyo aliwakaribisha vijana kutoka nchi za ulimwenguni kusini walioko kwenye fellowship, akisisitiza kuwa Misri inajivunia kuwa mwenyeji wa mipango inayokuza mchango wa vijana na kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa. Alielezea misingi ya sera ya mambo ya nje ya Misri, akisisitiza kuwa inatokana na mtazamo wa usawa na mkakati wa wazi ulioanzishwa na Rais Abdel Fattah El-Sisi tangu 2014. Alisisitiza kuwa Misri imejitolea kikamilifu kuunga mkono amani na utulivu katika eneo na dunia nzima kupitia diplomasia inayozingatia mazungumzo na suluhisho za amani.
Waziri alisisitiza imani ya Misri katika mfumo wa pande nyingi kama msingi wa mfumo wa haki wa kimataifa. Alisema Umoja wa Mataifa ni jukwaa lisiloweza kuepukika kwani linawakilisha matakwa ya pamoja ya jamii ya kimataifa. Pia alizungumzia ushiriki wa Misri katika taasisi za kimataifa, akisisitiza dhamira ya nchi hiyo kuleta mageuzi katika mfumo wa kimataifa, hususan katika Baraza la Usalama na mfumo wa kifedha wa kimataifa. Alisema kuwa hali ya sasa ya taasisi hizo haizingatii ipasavyo maslahi ya nchi za Kusini wala matarajio ya watu wake.
Katika muktadha huo, alielezea vipaumbele vya sera ya nje ya Misri kuhusu maendeleo endelevu, akitaja kuwa “Maoni ya Misri 2030” ni mfumo jumuishi unaozingatia usawa na kuwawezesha watu, sambamba na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Alionesha kuwa Misri ni kinara katika mabadiliko ya tabianchi, hasa baada ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa COP27, na kuanzisha mipango ya kusaidia mabadiliko ya kijani na ufadhili wa miradi ya mazingira katika nchi zinazoendelea, hasa zile za Afrika. Aliongeza kuwa teknolojia ya kidijitali na akili bandia ni nguzo muhimu za maendeleo ya siku zijazo, na Misri inaendelea kuvitumia kwa mujibu wa maslahi yake ya kitaifa.
Dkt. Abdel Aaty pia alizungumzia msimamo wa Misri kuhusu masuala ya eneo, akieleza kuwa ukanda huo unakumbwa na hali ya wasiwasi, huku misingi ya sheria za kimataifa ikiwa inapuuzwa. Alikemea ukiukaji wa sheria za kimataifa unaoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Wapalestina, na alilaani matumizi ya njaa kama silaha ya adhabu ya pamoja, jambo linalohatarisha usalama wa kimataifa na linahitaji hatua za haraka na madhubuti za jamii ya kimataifa kuheshimu sheria.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka washiriki wa Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa kushirikiana zaidi kama nchi za Kusini wa Dunia kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia leo. Alisisitiza kuwa njia ya kujenga mfumo wa haki wa kimataifa unaoheshimu mamlaka ya mataifa ni kushikamana na misingi ya sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kukataa kulazimisha matakwa kwa nguvu au kudhoofisha mamlaka ya mataifa. Alisema kuwa wakati huu unahitaji mshikamano thabiti wa nchi za Kusini ili kutetea haki na maslahi yao, na kuunda mfumo wa haki unaozingatia usawa na ushirikiano.
Kwa upande wake, Mtafiti wa Anthropolojia Hassan Ghazaly, mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa, alieleza kuwa washiriki wa Udhamini wa Uongozi wa Nasser wa Kimataifa walifanya ziara katika makao makuu ya serikali katika mji mkuu mpya wa kiutawala, ambapo walipata fursa ya kujionea kwa karibu mbinu za kazi za serikali ya Misri na uzoefu wake katika kutekeleza sera za umma na kufuatilia mipango ya maendeleo endelevu. Hili linaakisi mtazamo wa nchi wa kukuza uwazi na mawasiliano na vijana wa kimataifa. Aidha, washiriki walikutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhamiaji katika kikao chenye matokeo mazuri kilichozungumzia vipengele vya sera ya mambo ya nje ya Misri na nafasi yake muhimu katika kusaidia masuala ya nchi za Kusini mwa Dunia, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zisizofungamana na upande wowote. Hili liliwapa washiriki uelewa wa moja kwa moja na wa kina kuhusu mtazamo wa Misri katika maeneo ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia ya maendeleo, na kusaidia kuongeza uelewa wao kuhusu umuhimu wa uratibu kati ya viongozi vijana kukabiliana na changamoto za pamoja.
Hassan Ghazaly aliongeza kuwa kaulimbiu ya toleo la tano la Udhamini wa Uongozi wa Nasser wa Kimataifa inasisitiza juu ya uhusiano wa kimataifa kati ya Misri na Umoja wa Mataifa, katika kukabiliana na changamoto za Kusini mwa Dunia. Haya yanaenda sambamba na utekelezaji wa shughuli za maendeleo za Umoja wa Mataifa nchini Misri kwa kusaidia kutekeleza Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030, kwa namna inayolingana na Dira ya Misri 2030 na mikakati ya kitaifa ya sekta mbalimbali. Alibainisha kuwa msaada huu unalenga kufanikisha malengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na: Kuhamisha uzoefu wenye mafanikio kati ya nchi za Kusini mwa Dunia kuhusu uimara na ujenzi wa taasisi za kitaifa; Kutekeleza mbinu za ushirikiano wa Kusini kwa Kusini; Kuwahusisha vijana na wanawake katika ramani ya amani na usalama; Kuunda kizazi cha viongozi vijana kutoka nchi zisizofungamana na upande wowote, chenye mtazamo unaoendana na ushirikiano wa Kusini kwa Kusini; Na kufanya mtandao wa viongozi vijana wenye ushawishi mkubwa.
Ni vyema kutajwa kuwa toleo la kwanza la Udhamini huu lilitekelezwa mnamo Juni 2019, chini ya ufadhili wa Waziri Mkuu, kama sehemu ya juhudi za serikali ya Misri kuwawezesha vijana wa Afrika kwa mafunzo na nafasi za uongozi. Aliendelea kueleza kuwa msaada huu pia unatekelezwa sambamba na mpango wa Umoja wa Afrika wa mwaka 2021 wa kuwaandaa vijana milioni moja kwa uongozi, uliotangazwa na Rais Sisi wakati wa Jukwaa la Vijana Duniani (2018 na 2019). Toleo la pili, tatu na nne zilitekelezwa mnamo Juni 2021, 2022 na 2023 kwa udhamini wa Rais Abdel Fattah El-Sisi.