البحث

"Jukwaa la Kimataifa la Nasser" Laadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 80 Tangu Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Ushirikiano kati ya Misri na Umoja wa Mataifa

2025/05/14

Ziara katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Kikao cha Majadiliano Kuadhimisha Miaka 80 Tangu Kuanzishwa kwake.

Warsha maalumu kuhusu "Mitindo ya Uongozi" kandokando ya shughuli za siku ya nne ya toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa.

Kikao cha majadiliano chenye kichwa: "Misri na Umoja wa Mataifa – Miaka 80 ya Misingi na Ushirikiano" katika hitimisho la shughuli za siku ya nne za Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa.

Jukwaa la Nasser la Kimataifa liliongeza katika taarifa yake kuwa, kandokando ya ziara hiyo, lilifanyika kikao cha majadiliano kuadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kwa kuhudhuriwa na Waziri Mshauri Faisal Ali Gassal, Mkurugenzi wa Idara ya Vijana na Michezo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, pamoja na viongozi kadhaa kutoka Wizara ya Vijana na Michezo wakiongozwa na Meja Jenerali Ismail Al-Far, Msaidizi Mkuu wa Waziri wa Vijana na Michezo, na Alaa El-Dessouky, Naibu Waziri na Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Vijana, pamoja na Hassan Ghazaly, Mwanzilishi wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa, ambaye ndiye aliyeongoza kikao hicho muhimu cha majadiliano. Katika mwanzo wa hotuba yake, Ghazaly alieleza kuwa kikao hiki cha majadiliano kimekuja sambamba na maadhimisho ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kutimiza miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ndiyo taasisi ya kwanza ya kikanda kuanzishwa hata kabla ya Umoja wa Mataifa.

Hapo awali, Waziri Mwandamizi Mteule Faisal Ali Ghsal, Mkurugenzi wa Idara ya Vijana na Michezo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, aliwakaribisha washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa. Alieleza furaha yake kwa uwepo wao katika makao makuu ya Jumuiya ya Kiarabu, “nyumba ya Waarabu wote”, hasa katika Jiji la Kairo, ambako tamaduni mbalimbali zinachanganyika na kuifanya kuwa jiji la kihistoria lenye mizizi ya kale. Alisema kuwa hali hii imeifanya Kairo kuwa mahali muafaka kwa makao ya moja ya mashirika ya kikanda ya zamani zaidi duniani. Ghsal alieleza kuwa ushiriki wa vijana hao unakuja katika tukio la kipekee, kwani Jumuiya ya Kiarabu inasherehekea miaka 80 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1945, wakati ambapo nchi saba za Kiarabu zilikutana kwa lengo moja – kujikomboa kutoka kwa ukoloni na kuimarisha mshikamano wa Kiarabu – ili kuifanya Jumuiya hiyo kuwa sauti ya mataifa ya Kiarabu na jukwaa la ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Aliongeza kuwa Jumuiya ya Kiarabu siyo tu mahali pa mikutano ya kisiasa, bali pia inatekeleza malengo yake kwa kuimarisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kuhakikisha amani na usalama. Alisisitiza dhamira ya kudumu ya Jumuiya hiyo katika kuunga mkono masuala ya haki kwa mataifa ya Kiarabu, likiwemo kwa kipaumbele cha juu suala la Palestina, ambalo bado ni alama ya azimio na uvumilivu, Akiisifu misimamo thabiti ya watu wa Palestina na kusema kuwa Palestina imewafundisha wengi kuwa heshima haibadilishwi kwa chochote na haki haiwezi kusahaulika hata kama muda utapita. Alitoa salamu za heshima kwa watu wa Palestina, akawaombea mashujaa waliopoteza maisha rehema, na kutakia kuondoka kwa giza hili hivi karibuni.

Katika hotuba yake kwa washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, Mkurugenzi wa Idara ya Vijana na Michezo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu aliwasilisha kwa njia ya maonyesho ya kina historia ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kiarabu na mchango wake mkuu katika kuinua ustawi wa ulimwengu wa Kiarabu kwa kipindi cha miaka 80, ikizingatiwa kuwa ndiyo taasisi ya kwanza ya kikanda ya Kiarabu katika historia ya kisasa. Alieleza kuwa Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi wanachama, kuratibu mipango yao ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, pamoja na kushughulikia masuala ya usalama wa pamoja wa Kiarabu na changamoto zinazotishia uthabiti wa eneo hilo.

Alisisitiza kuwa tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1945, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imekuwa ikitekeleza jukumu muhimu katika kuimarisha mshikamano wa Kiarabu, kuunga mkono umoja wa mataifa ya Kiarabu, na kutatua migogoro kupitia mazungumzo na maridhiano. Pia alizungumzia Mkataba wa Jumuiya ya Kiarabu unaotoa mwongozo wa kazi za Jumuiya hiyo, akieleza pia kuhusu vyombo mbalimbali vya Jumuiya ambavyo ni: Baraza la Jumuiya, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, mabaraza ya mawaziri ya kisekta, Sekretarieti Kuu, pamoja na mashirika maalumu ya Kiarabu na Bunge la Kiarabu. Alifafanua kuwa miundo hiyo ya kitaasisi ndiyo msingi wa utendaji kazi wa Jumuiya kwa ajili ya kufikia malengo yake na kuimarisha ushirikiano wa Kiarabu, kwa namna inayolingana na mabadiliko ya dunia ya sasa na matamanio ya wananchi wa Kiarabu katika maendeleo na uthabiti.

Washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa walijadili katika kikao cha majadiliano kilichoandaliwa pembezoni mwa ziara yao katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, pamoja na Mjumbe Mwandamizi Bwana Faisal Ali Ghassal, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Vijana na Michezo katika Jumuiya hiyo, kuhusu masuala na mada nyingi muhimu zinazojitokeza katika ulingo wa Kiarabu na kimataifa. Pia walizungumzia mbinu na mikakati ya utekelezaji inayotumika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokumba nchi nyingi za Kiarabu, pamoja na kujadili kwa kina nafasi ya Jumuiya hiyo katika kuunga mkono suala la Palestina na jinsi ya kuimarisha ushiriki wa Waarabu katika jukwaa la kimataifa.

Baada ya majadiliano, maafisa wa mapokezi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu waliwasindikiza viongozi hao vijana walioko chini ya Udhamini wa Nasser kutembelea sehemu mbalimbali za makao makuu ya Jumuiya na kujifunza kuhusu idara zake tofauti. Ziara hiyo ilihitimishwa kwa washiriki kupiga picha nyingi za kumbukumbu wakiwa wamejaa furaha na heshima ya kuwepo ndani ya taasisi hii kongwe na yenye mchango mkubwa katika ulimwengu wa Kiarabu. Kwa upande wake, Meja Jenerali Ismail El-Far, Msaidizi Mkuu wa Waziri wa Vijana na Michezo, alisifu taarifa muhimu na zenye thamani kubwa walizozipata washiriki kuhusu historia ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na mafanikio yake katika kuleta umoja miongoni mwa nchi za Kiarabu, kuimarisha mahusiano kati yao, na mchango wake katika ngazi ya Kiarabu na kimataifa. Alisisitiza kuwa ziara ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni miongoni mwa matukio muhimu zaidi katika programu ya toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, ambalo limewaleta pamoja viongozi vijana 150 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mwanzoni mwa hotuba yake, Bw. Alaa El-Dessouky, Naibu Waziri na Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Vijana, alitoa shukrani kwa viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa mapokezi yao ya kipekee kwa washiriki wa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, akieleza furaha yake kwa jinsi washiriki walivyoshiriki kwa ari kubwa katika kikao hicho cha majadiliano kilichoandaliwa sambamba na maadhimisho ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Warsha Maalum Kuhusu “Mitindo ya Uongozi” Pembeni mwa Matukio ya Siku ya Nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa – Toleo la Tano

Katika taarifa yake rasmi, Jukwaa la Nasser la Kimataifa lilieleza kuwa matukio ya siku ya nne ya toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa yalijumuisha pia kuandaliwa kwa warsha maalumu kuhusu mitindo ya uongozi,  iliyolenga kuwasaidia vijana kutambua mbinu mbalimbali za uongozi kupitia hali halisi na michezo ya kuigiza. Washiriki walifahamishwa kuhusu mitindo tofauti ya uongozi, ikiwemo: uongozi wa maamuzi ya haraka na thabiti, uongozi unaohimiza ushirikishwaji na majadiliano, mtindo unaotoa uhuru kwa timu kufanya maamuzi yao wenyewe, na ule unaojikita katika kukuza, kuelekeza na kutoa msaada. Kupitia warsha hiyo, washiriki walijaribu mitindo hii katika hali za kiigizo ili kujifunza ni wakati gani kila mtindo unafaa zaidi – kama vile uongozi wa maamuzi kwa nyakati za dharura, uongozi shirikishi kwa timu za ubunifu, na uongozi wa msaada kwa timu zilizo katika hatua ya kujifunza au kujijenga.

Lengo kuu la warsha lilikuwa kuwasaidia washiriki kila mmoja kupata uelewa wa kina wa mtindo wake binafsi wa uongozi na namna ya kuuendeleza kulingana na watu, mazingira na changamoto wanazokutana nazo. Warsha hiyo iliendeshwa na timu mahiri ya wawezeshaji walioteuliwa kutoka miongoni mwa wahitimu wa awamu zilizopita za Udhamini wa Nasser, wakiwemo: Dkt. Ahmed Mokhtar (mhitimu wa Kundi la Pili), Dkt. Rajaa Magdy (Mhitimu wa Kundi la Nne), na Dkt. Rasha Hussein (Mhitimu wa Shule ya Afrika). Kwa kutumia uzoefu wao mpana na wa kipekee, timu hii ya wakufunzi ilijitahidi kuunga mkono malengo ya udhamini na kuchangia kikamilifu katika kuwawezesha washiriki kukuza ujuzi wao wa kiuongozi na binafsi, pamoja na kuimarisha uwezo wao ndani ya mazingira ya kimataifa yenye utofauti wa kitamaduni, kwa lengo la kujenga kizazi cha viongozi vijana waliokomaa na wenye ushawishi chanya.

Kikao cha Majadiliano chenye kichwa: “Misri na Umoja wa Mataifa – Miaka 80 ya Msingi na Ushirikiano” katika Hitimisho la Matukio ya Siku ya Nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa

Kwa mujibu wa taarifa ya Jukwaa la Nasser la Kimataifa, matukio ya siku ya nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa katika toleo lake la tano, linalofanyika mwezi Mei huu chini ya kaulimbiu: “Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi wa Masuala ya Ulimwenguni Kusini”, yalihitimishwa kwa kikao cha majadiliano kilichobeba kichwa: “Misri na Umoja wa Mataifa – Miaka 80 ya Msingi na Ushirikiano”, chini ya Ufadhili rasmi wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri. Taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho cha majadiliano, kilichokuwa miongoni mwa matukio muhimu ya siku ya nne ya udhamini, kiliwaleta pamoja wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nchini Misri, wakiwemo: Yves Sassenrath, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini Misri, na Ahmed Rizk, Mkurugenzi wa Mpango wa Makazi wa Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) nchini Misri, na Natalia Winder-Rossi, Mwakilishi wa UNICEF nchini Misri na Marwa Alameldin, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) nchini Misri. Kikao hicho kiliongozwa na Salma Tawfiq, Mhitimu wa Kundi la nne la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, aliyesimamia mjadala kwa umahiri mkubwa, ukisisitiza ushirikiano wa kihistoria na wa kimkakati kati ya Misri na Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miongo minane iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jukwaa la Nasser la Kimataifa, Yves Sassenrath, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini Misri, alieleza katika hotuba yake wakati wa kikao cha majadiliano cha kuhitimisha matukio ya siku ya nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, umuhimu wa kushughulikia masuala ya idadi ya watu pamoja na fursa zilizopo katika ukanda huu, Alisisitiza juu ya jukumu la Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono afya ya wanawake tangu kuzaliwa hadi hatua mbalimbali za maisha, akitaja hitaji la kuchukua hatua madhubuti ili kuendeleza afya ya wanawake kiakili, kisaikolojia na kimwili, pamoja na kuimarisha afya ya uzazi.

Aidha, alieleza umuhimu wa kuwawezesha vijana wa kizazi kipya, kuimarisha uwezo wao, na kuzingatia afya yao ya uzazi na ya kifamilia. Sassenrath alitambua kuwa vijana ndio nguzo kuu ya mpango huu, na akatoa wito wa kuunda mazingira yatakayowawezesha watu wote kufanya maamuzi ya msingi kwa uelewa, pamoja na kuwapa fursa ya kuwa na athari chanya katika jamii zao, Akiongeza kuwa vijana kwa sasa wana fursa nyingi na njia za kuwasiliana na jamii kupitia mradi huu muhimu unaoanzishwa na Misri.

Aidha, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini Misri alisisitiza katika hotuba yake kuhusu umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho na maamuzi ya haraka katika muktadha wa dunia unaobadilika kwa kasi, sambamba na maendeleo ya akili bandia (AI), na namna ya kushinda changamoto za jadi na mila zilizopitwa na wakati ambazo huzuia mabadiliko. Alibainisha kuwa mabadiliko huanzia ndani ya mtu binafsi kabla ya kusambaa kwa wengine, akisisitiza umuhimu wa mawasiliano miongoni mwa wanajamii. Sassenrath alitoa wito wa kuwapa vijana nafasi, nyenzo, na njia mbalimbali za kuwasiliana na jamii zao, akisisitiza kuwa wao ndio viongozi wa baadaye. Aliongeza kuwa utamaduni ni mojawapo ya njia kuu za mawasiliano kati ya watu. Pia alisisitiza kuhusu msimamo wa kutokuwa na upendeleo wa Umoja wa Mataifa na uwezo wake wa kuwasiliana na kila mtu kwa usawa, akitoa nafasi kwa vijana kupanda hadi ngazi ya kimataifa na kuanzisha mifumo rafiki kwa vijana inayofaa mazingira yao.

Ahmed Rizk, Mkurugenzi wa Mpango wa Makazi wa Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) nchini Misri, alieleza katika hotuba yake kwa washiriki wa Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa kuwa shirika hilo linaweka mkazo katika kujenga jamii endelevu na hutoa msaada kwa nchi wanachama ili kufanikisha maendeleo endelevu, hasa katika nyanja ya maendeleo ya miji, ambayo inaingiliana kwa kiwango kikubwa na nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku. Alisisitiza kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya upangaji miji na afya ya watu, na kwamba kuna mfumo wa kimkakati unaosimamia masharti, usanifu, upangaji na ufadhili wa miradi ya maendeleo ya miji. Aidha, alitoa wito wa kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali, pamoja na kuunda ajenda ya maendeleo ya miji itakayobainisha aina ya ushirikiano kati ya nchi zinazotekeleza miradi ya maendeleo ya miji, huku ikizingatia mipango ya miji nchini Misri na muunganiko kati ya maeneo ya vijijini na kilimo.

Rizk alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kufuata viwango vya kisayansi na kuepuka ubaguzi katika eneo la usanifu na mipango miji. Alibainisha pia umuhimu wa mchango wa vijana na mshikamano wao katika miji midogo, na uwezo wao wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana katika jamii. Mwisho, alithibitisha kuwa Misri ina fursa nyingi zinazotolewa na Umoja wa Mataifa pamoja na sekta ya kiraia kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwa ufanisi zaidi katika siku zijazo.

Kwa upande wake, Natalia Winder Rossi, Mwakilishi wa UNICEF nchini Misri, alieleza katika hotuba yake wakati wa kikao cha mwisho cha siku ya nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, kuhusu furaha yake ya kushiriki katika tukio hili muhimu. Alibainisha kuwa UNICEF imekuwa ikifanya kazi nchini Misri tangu mwaka 1996 kwa ajili ya kulinda watoto na kuhakikisha wanapata fursa sawa za kukua na kustawi ndani ya jamii.
Alisisitiza kuwa serikali, mashirika na wadau mbalimbali katika mikoa yote ya Misri wanaonyesha juhudi kubwa za kujumuisha watoto na vijana, ambao ni rasilimali kuu ya taifa, akisisitiza kuwa huu ni wakati mwafaka wa kuwekeza kwao kupitia mifumo ya kijamii inayowalinda na kuwapa kipaumbele. Natalia alieleza kuwa UNICEF ina programu jumuishi za elimu zinazolenga kuhakikisha kuwa watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanahusishwa ipasavyo, kwa ushirikiano na wadau husika ili kufanikisha malengo haya. Aidha, alizungumzia juhudi za shirika hilo za kulinda watoto dhidi ya unyonyaji, kupambana na ndoa za utotoni, ujauzito wa mapema, na kuhakikisha afya bora ya akili kwa watoto. Aliongeza kuwa vipaumbele vya UNICEF kwa sasa ni pamoja na kuwezesha vijana, kuimarisha ushiriki wao, kuwapa ujuzi, kuwaandaa kitaaluma, na kuhakikisha programu mbalimbali zinawafikia walengwa kwa ushirikiano na washirika, hasa Wizara ya Vijana na Michezo, kwa lengo la kuunda mfumo wa usawa wa fursa kwa wote.

Pia alisisitiza kuwa haiwezekani kuunda sera kwa ajili ya watoto bila kushirikisha vijana, kuwasikiliza, na kutafuta suluhisho bora kwa changamoto zao. Alionyesha umuhimu wa mawasiliano bora na watoto, vijana, na balehe ili kuelewa mahitaji yao na kutumia uwezo wao mkubwa wa kutumia teknolojia ya mtandao. Mwisho, alibainisha dhamira ya UNICEF ya kuendeleza njia bora za kazi, kuchangia katika kupanga mipango yenye malengo makubwa, na kuzingatia kuunda mazingira salama na yenye msaada kwa ubunifu, ili kufanikisha athari halisi kupitia mawazo yanayobadilisha jamii.

Marwa Alameldin, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Masuala ya Wanawake nchini Misri, alisisitiza katika hotuba yake wakati wa kikao cha mwisho cha siku ya nne ya Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, umuhimu wa kufanikisha usawa wa kijinsia, akieleza kuwa wanawake si waathirika tu wa migogoro, bali ni nguzo kuu ya amani. Alibainisha kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi nchini Misri kwa takriban miaka 25, likishughulikia masuala ya wanawake na likitoa mratibu wa huduma za ushauri kwa wanawake na wanaume kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa. Pia alithibitisha kujitoa kwao katika kufanikisha usawa wa kijinsia, pamoja na kufanya kazi kwa karibu na mashirika ya kimataifa yanayopinga unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Marwa alieleza kuwa kazi ya shirika nchini Misri inazingatia nguzo kuu tatu:
• Uongozi na uwezeshaji wa wanawake na wasichana kwa kuwapa ujuzi wa kitaalamu na kuwasaidia kupata huduma kwa haraka na kwa urahisi.
• Uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake, kwa kuunda mazingira rafiki ya ajira, kuwapatia fursa za kiuchumi, na kuunga mkono miradi yao binafsi.
• Kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake kwa kuzuia, kukabiliana nao, na kuhakikisha usalama katika sehemu za kazi, usafiri, na maeneo ya umma.

Alisisitiza kuwa nguzo hizi tatu zinahusiana kwa karibu na hujengwa juu ya msingi wa kusaidiana. Aidha, alieleza kuwa wanawake nchini Misri, iwe ni wakazi wa kudumu au wakimbizi, wanapatiwa huduma na fursa nyingi zinazolenga kuhakikisha usalama wao wa kijamii na kijinsia. Pia aliwasilisha baadhi ya mifano ya programu na miradi yenye mafanikio, ikiwemo mpango wa Rabha na mafunzo mengine yaliyotolewa katika mikoa mbalimbali ya Misri, na alihimiza umuhimu wa kudumisha vipengele vya mafanikio katika juhudi hizi ili kuendeleza mabadiliko chanya kwa wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jukwaa la Nasser la Kimataifa, katika hitimisho la kikao cha majadiliano cha toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, washiriki walitoa maswali mengi kuhusu masuala mbalimbali, yakiwemo unyanyasaji dhidi ya wanawake na mbinu bora za kuukabili, pamoja na changamoto nyingine zinazowakumba wanawake, ikiwemo afya ya uzazi.
Vilevile, washiriki waliuliza kuhusu mashirika ya upangaji miji na miradi mikubwa nchini Misri kama vile mji mkuu mpya wa kiutawala, na jinsi ya kuhakikisha miradi hiyo ni endelevu, sambamba na maendeleo yaliyoiwezesha Misri kuwa kiongozi katika sekta hiyo. Majadiliano pia yaligusia safari ya uwekezaji na maendeleo ya miji mipya ya Alamein, kama sehemu ya mpango mpana wa pande nyingi unaojumuisha ushirikiano na wadau mbalimbali, na mchango wake katika kuendeleza maeneo yanayozunguka miji hiyo. Aidha, washiriki walijadili pia suala la makazi bora, uendelezaji wa miundombinu, na kuboresha viwango vya maisha na huduma zinazopatikana, kwa lengo la kuhakikisha makazi bora na maisha ya kiwango cha juu kwa raia katika nchi mbalimbali.

أخبار ذات صلة: