البحث

Hitimisho la toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa kwa uwepo wa Waziri wa Vijana na Michezo

2025/05/28

Jukwaa la Nasser la Kimataifa limetangaza kupitia taarifa yake rasmi kuhusu kuandaliwa kwa sherehe ya kufunga rasmi Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa kwa heshima ya kiongozi wa kihistoria hayati Gamal Abdel Nasser, katika toleo lake la tano, uliofanyika chini ya Ufadhili wa Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Misri, na kwa ushirikiano madhubuti na Umoja wa Mataifa, chini ya kaulimbiu: “Misri na Umoja wa Mataifa: Miaka 80 ya Uwakilishi wa Masuala ya Ulimwenguni Kusini ”. Udhamini huu ulifanyika kuanzia tarehe 10 hadi 25 Mei mwaka huu, kwa ushiriki wa vijana 150 viongozi kutoka nchi 80 duniani, wakiwa ni kutoka nyanja mbalimbali za utekelezaji sera, mashirika ya kiraia, na vijana wenye ushawishi katika maamuzi.

Sherehe ya kufunga toleo hili la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa ilihudhuriwa na Dkt. Ashraf Sobhy, Waziri wa Vijana na Michezo, pamoja na mabalozi wa nchi shiriki, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake yanayofanya kazi nchini Misri, wawakilishi wa taasisi za kitaifa na kimataifa, pamoja na watu mashuhuri katika jamii, viongozi wa Wizara ya Vijana na Michezo, waandishi wa habari na wanahabari. Uwepo huu wa ngazi ya juu unadhihirisha umuhimu wa fursa hii kama jukwaa la kimataifa linalojumuisha tamaduni mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mazungumzo baina ya tamaduni duniani.

Sherehe ya kufunga rasmi toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa ilianza kwa kuimbwa wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, ikifuatiwa na maonesho mbalimbali ya sanaa yaliyodhihirisha utajiri na utofauti wa tamaduni za nchi shiriki, jambo lililoongeza hali ya shangwe na furaha katika ukumbi wa hafla. Ukumbi wa sherehe ulijaa hisia za furaha na fahari, huku washiriki wa fursa hiyo wakionyesha hamasa kubwa walipokuwa wakishiriki nyimbo na maonesho yaliyotolewa. Wengi wao walieleza furaha yao kwa kushiriki katika uzoefu huu wa kipekee wa uongozi. Hisia za kujivunia na kutambulika zilionekana wazi katika kipindi cha kuhitimu, kilichokuwa kilele cha safari ya kujifunza na kubadilishana tamaduni. Washiriki walieleza kwa moyo wa shukrani fursa waliyopewa ya kujenga mahusiano na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa mbalimbali duniani.

Katika hotuba yake pembezoni mwa sherehe ya kufunga, Waziri wa Vijana na Michezo Dkt. Ashraf Sobhy alieleza furaha yake kukutana na washiriki katika hitimisho la toleo hili maalumu la fursa, akisisitiza kuwa udhamini wa Rais kwa fursa hii unaakisi imani ya uongozi wa kisiasa katika nafasi muhimu ya vijana, na kujitolea kwa dola ya Misri kuendeleza na kuimarisha uwezo wa vijana kitaifa na kimataifa. Waziri alifafanua kuwa Udhamini wa Nasser kwa Uongozi ni mfano hai wa ushirikiano wa kimataifa na mazungumzo yenye kujenga, kwani imekusanya vijana 150 kutoka nchi 80 katika uzoefu wa kipekee unaoonesha utofauti wa kitamaduni na mtazamo wa wazi kwa ulimwengu. Aidha, alisisitiza dhamira ya Misri ya kujenga madaraja ya ushirikiano na nchi za Kusini, pamoja na kuwekeza katika uwezo wa vijana na kuwawezesha kutekeleza majukumu yenye athari katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Alisifu pia wahitimu wa Jukwaa la Nasser la Kimataifa kwa uongozi kwa namna walivyoonyesha weledi na ustadi ulioendana na uzoefu walioupata wakati wa fursa.

Katika mazungumzo yake katika sherehe ya kufunga toleo la tano, Waziri wa Vijana na Michezo alieleza kuwa shughuli mbalimbali zilizofanyika katika fursa hiyo – ikiwemo vikao shirikishi na ziara za kielimu – zililenga kuwasilisha uzoefu wa Misri katika kujenga taasisi za kitaifa na kuimarisha kazi za kijamii, hasa katika maeneo ya kuwawezesha vijana na wanawake. Alisisitiza kuwa fursa hiyo imetoa mfano wa uongozi wa kuigwa unaojengwa kuhusu ushirikiano badala ya utegemezi, na juu ya utofauti badala ya migongano. Dkt. Sobhy alithibitisha kuwa Wizara ya Vijana na Michezo, kwa mwongozo wa uongozi wa juu, itaendelea kuunga mkono mipango yote inayochangia kuimarisha uwezo wa vijana na kuwawezesha kuwa na nafasi madhubuti katika jamii zao. Alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa washirika wote wa kitaifa na kimataifa kwa msaada wao endelevu, akieleza matarajio yake ya kukutana tena na washiriki katika toleo lijalo la fursa hapa nchini Misri, ili kuendeleza safari ya ujenzi na ushirikiano kwa ajili ya dunia yenye haki na amani zaidi. Alimaliza hotuba yake kwa kusema: "Idumu Misri... na Idumu mataifa ya dunia kwa amani na maendeleo."

Kwa upande wake, Yves Sassenrath, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini Misri, alieleza katika hotuba yake kuwa ujumbe wa vijana ulioshiriki katika toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, unaonesha kuwa udhamini huu hauko tena kama jukwaa la mafunzo pekee, bali umekuwa alama hai ya ushirikiano baina ya nchi za Kusini, na mfano wa dhahiri wa ushirikiano wa kidiplomasia unaoongozwa na vijana. Aliongeza kuwa udhamini wa Nasser unaakisi nafasi ya uongozi inayochukuliwa na Misri katika kuunda kizazi kinachotambua changamoto za dunia, na kilicho tayari kukabiliana nazo kwa ujasiri na dhamira thabiti kupitia maono ya pamoja ya dunia yanayojengwa juu ya mshikamano, usawa na ushirikiano kwa ajili ya mustakabali endelevu na wa haki zaidi.

Naye Hassan Ghazaly, Mwanzilishi wa Jukwaa la Kimataifa la Nasser, alielezea katika hotuba yake kwenye sherehe ya kufunga toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi wa Kimataifa, kuwa Udhamini huu ulianza miaka sita iliyopita na umeendelea kufanikishwa kwa msaada mkubwa kutoka kwa Dkt. Ashraf Sobhy, Waziri wa Vijana na Michezo, ambaye ndiye alikuwa mhamasishaji mkuu wa kuzinduliwa kwa mpango huu licha ya changamoto zilizokuwepo. Ghazaly alieleza kuwa udhamini huo ulihusisha mfululizo wa vipindi vya mafunzo, mijadala ya wazi, warsha, na ziara mbalimbali za kimkakati kwa lengo la kuwawezesha washiriki kupata ujuzi wa uongozi wenye tija na athari katika jamii zao. Aidha, alibainisha kuwa sherehe ya kufunga ilifanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Afrika, tukio linaloonesha roho ya mshikamano miongoni mwa mataifa ya bara hilo. Alimaliza hotuba yake kwa kutoa shukrani kwa wenzake katika Wizara ya Vijana na Michezo na timu nzima ya kazi waliotoa juhudi kubwa kufanikisha toleo hili, pamoja na ujumbe wa vijana wa Misri waliotoa uwakilishi wa kipekee.

Katika sherehe ya kufunga Udhamini wa Nasser kwa Uongozi – Toleo la Tano, Waziri wa Vijana na Michezo Dkt. Ashraf Sobhy alitoa tuzo za heshima kwa baadhi ya washirika, wadhamini na washiriki waliobobea katika toleo hili. Miongoni mwa waliotunukiwa ni: Waziri wa zamani wa mambo ya nje na habari Mohamed Faeeq ambaye pia alikuwa muhimili wa harakati za ukombozi barani Afrika (tuzo ilipokelewa kwa niaba yake na mjukuu wake Ali Faeeq), Heba Rashid – Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mersal na mshiriki wa muungano wa kitaifa, Asmaa Al-Husseini – mwandishi na mhariri mkuu wa gazeti la Al-Ahram na mwanachama wa Baraza la Misri la Masuala ya Kigeni, Iman Al-Warraqi – mwandishi wa uchunguzi na mwanzilishi wa Mpango wa Mapinduzi ya Akili Bandia, Sherif Gad – Mkurugenzi wa shughuli za kitamaduni katika Kituo cha Utamaduni cha Urusi, Dkt. Ahmed Mokhtar – mtaalamu wa midahalo na ujenzi wa uwezo, Dkt. Bassem El-Maghraby – mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Suez Canal, Dkt. Ragaa Magdy – mratibu wa shughuli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ahram Canadian, Dkt. Rasha Hussein El-Sayed – mshauri katika Ofisi ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale na mhitimu wa Shule ya Afrika 2063, Said Fouad – Rais wa Tamasha la Filamu la Luxor la Afrika, Mariam Allam – Mkuu wa Timu ya Mabadiliko ya Tabianchi na mshauri wa urais katika Mkutano wa COP27, Dkt. Shaimaa Tarek – Msaidizi wa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ain Shams, mratibu wa mafunzo ya mabalozi wa Jukwaa la Nasser, na Mchunguzi Yasmin Mahmoud – Mratibu wa Ukanda wa Afrika Mashariki na wa kijiografia wa Jukwaa la Nasser, na Mchunguzi Mervat Sakr – Mratibu wa lugha ya Kiswahili wa Jukwaa la Nasser na Mtandao wa Mshikamano wa Kimataifa, na Mchunguzi Hanan Sobhy – Mratibu wa Ukanda wa Afrika Kaskazini wa Jukwaa la Nasser, na wasanii Ahmed Zaher na Mohamed Adel.

Sherehe ya kufunga Toleo la Tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi ilihitimishwa kwa kugawa vyeti vya kutambua ushiriki kwa wajumbe wa mataifa mbalimbali walioshiriki. Dkt. Ashraf Sobhy, Waziri wa Vijana na Michezo, aliwakabidhi vyeti hivyo katika mazingira yaliyojaa furaha na fahari. Washiriki walieleza furaha yao kubwa kwa kushiriki katika uzoefu huu wa kipekee uliowapa fursa ya kujifunza, kujadiliana, na kupata maarifa ya vitendo na ya kinadharia katika nyanja za uongozi, kazi ya kijamii, na diplomasia ya vijana. Washiriki wengi walionesha kuvutiwa sana na kiwango cha maandalizi na maudhui ya kielimu na kiutamaduni yaliyotolewa katika udhamini huu, wakisisitiza kuwa ilikuwa ni jukwaa halisi la kubadilishana mawazo na kuimarisha ushirikiano baina ya vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani. Pia walitoa shukrani kwa fursa ya kuwasiliana na kujenga urafiki mpya na vijana kutoka asili na tamaduni tofauti. Walipiga picha na kurekodi video nyingi kama kumbukumbu ya nyakati hizi maalumu, wakithibitisha kuwa tukio hili litaendelea kubaki katika kumbukumbu zao na litakuwa ni motisha ya kuendeleza kazi ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

Ni vyema kutajwa kuwa toleo la tano la Udhamini wa Nasser kwa Uongozi lililenga hasa kuwasilisha uzoefu wa kipekee wa Misri katika kujenga taasisi za kitaifa zenye uimara, kukuza mazungumzo miongoni mwa vijana katika ngazi ya kimataifa, na kuangazia nafasi ya wanawake na vijana katika masuala ya amani, usalama na kazi za kujitolea. Aidha, lililenga kuangazia masuala yanayowakabili vijana, changamoto za nchi za Kusini na ushirikiano wa Kusini-Kusini, pamoja na kuwaelimisha vijana kuhusu nafasi ya Umoja wa Mataifa na mchango wake katika kushughulikia masuala ya nchi za Kusini, sambamba na kuonesha nafasi ya nchi za Kusini katika kusaidia ajenda muhimu za nchi zinazoendelea na kuimarisha haki ya kimataifa.

أخبار ذات صلة: